Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Dawud Fazil Falawirjani, mjumbe wa baraza la utafiti la Taasisi ya Imam Khomeini (r.a), katika mahojiano na mwandishi wa Habari za Hawza, alichambua hali ya Venezuela na kusema: Kwa miezi kadhaa sasa, Marekani kwa kisingizio cha kupambana na usafirishaji wa dawa za kulevya imetuma meli zake hadi pwani za Karayib na inadai kuwa mtandao wa dawa za kulevya hutumia njia hii kuziingiza Marekani; ilhali tunafahamu wazi kwamba hatua hii ni kisingizio tu cha kutekeleza malengo ya kisiasa ya Washington.
Mjumbe wa baraza hilo, akibainisha umuhimu wa kimkakati wa Venezuela huko Amerika ya Kusini, aliongeza: Katika karne iliyopita, bara la Amerika ya Kusini chini ya Daktirini ya Monroe lilifafanuliwa kama "eneo la nyuma la Marekani”; eneo ambalo Marekani ililiona kama sehemu ya nyumba yake na haikuruhusu nguvu nyingine kuingilia. Katika muktadha huo, eneo la Karayib ni nyeti sana kijiografia na lina visiwa vingi vyenye umuhimu mkubwa, ikiwemo Cuba – kisiwa kilicho karibu mno na Marekani kiasi kwamba kutoka huko hadi Miami au majimbo ya kusini mwa Marekani hakuna umbali mkubwa. Zaidi ya hayo, mataifa mengi katika eneo hili huzungumza Kihispania, na iwapo nchi hizo zitapata nguvu, zinaweza kuathiri siasa za ndani za Marekani.
Akasema: Ugunduzi wa rasilimali kubwa za mafuta nchini Venezuela katika miaka ya hivi karibuni umeongeza umuhimu wa nchi hiyo mara dufu; hivi sasa Venezuela ina kiwango cha juu zaidi cha akiba ya mafuta duniani. Zaidi ya hayo, Venezuela na nchi jirani kama Colombia zina rasilimali nyingi za asili na ndiyo vinakopatikana vito bora zaidi vya zumaridi duniani. Uwezo huu umeigeuza Venezuela kuwa sehemu muhimu sana katika mahesabu ya kimkakati ya Marekani.
Hujjatul-Islam Fazil Falawirjani, akirejea nafasi ya Hugo Chávez, alisema: Alipoingia madarakani, kutokana na sera zake za kupinga Marekani na uhusiano wake na Iran na Urusi, Chávez aligeuka kuwa tishio kubwa kwa Marekani kiasi kwamba walijaribu kumwangamiza kwa njia ya “shambulio la kibayolojia”. Baada ya Chávez, alipoingia Nicolás Maduro, Marekani ilidhani ingeweza kuiangusha serikali ya Venezuela kwa urahisi, na tangu 2017 ikaweka vikwazo vikali sana dhidi ya nchi hiyo kiasi kwamba thamani ya sarafu ya Venezuela ilidorora mno na kuwa haina thamani.
Aliongeza: Baada ya kushindwa kwa mbinu ya vikwazo, Marekani chini ya serikali ya Trump ilichagua mbinu ya vitisho vya moja kwa moja; kuanzia kutishia kukamatwa kwa rais wa Venezuela hadi kutangaza zawadi ya mamilioni ya dola kwa yeyote atakayemkamata. Lakini hatua hizo hazikufanikiwa. Hatimaye Washington ikaamua kuanzisha vita vya kisaikolojia kwa kueneza hofu ya shambulio la kijeshi na kuweka meli za kivita, kwa lengo la kuitikisa serikali ya Venezuela kutoka ndani. Vita hivi vya kisaikolojia vilikuwa vikubwa kiasi cha kwamba hata baadhi ya watu nchini Iran – wakichochewa na vyombo vya habari – walisambaza taarifa za hali mbaya ilhali raia wa Venezuela waliendelea na maisha yao ya kawaida. Lengo la Marekani lilikuwa kuunda hofu ya shambulio la karibu ili kulisukuma taifa hilo kuelekea kuporomoka; lakini mpango huu pia ulishindwa, na Venezuela ikaweza kushikilia msimamo wake.
Changamoto za Marekani huko Karayib na uwezekano wa matukio kuhusu Venezuela
Mjumbe wa baraza la utafiti la Taasisi ya Imam Khomeini (r.a), akieleza thamani ya kijiografia ya Venezuela na uzoefu wa kimashinani nchini humo, alisema kwamba hatua za karibuni za Marekani katika Karayib ni sehemu ya “shambulio kubwa la kisaikolojia” lenye lengo la kuiyumbisha serikali ya Caracas, na akasisitiza: Kuingilia moja kwa moja kutakuwa na gharama kubwa na matokeo yasiyotabirika kwa Washington. Alisema: Katika kipindi cha miaka 100 iliyopita, Marekani haijawahi kuvamia moja kwa moja kijeshi huko Amerika ya Kusini; imekuwa ikitumia mapinduzi ya kuongozwa kisiasa, na katika Venezuela pia walijaribu mara nyingi kufanya mapinduzi.
Kuhusu uwezekano wa uvamizi wa moja kwa moja, alisema: Marekani ina wasiwasi kuhusu mambo mawili makubwa; kwanza, mazingira magumu ya kijiografia ya Venezuela na uwepo wa magenge ya kimafia ambayo yanaweza kuigeuza operesheni ya kijeshi kuwa tope, na kuifanya Venezuela kuwa Syria au Libya mpya – lakini safari hii karibu kabisa na ardhi ya Marekani; pili, iwapo shambulio litafanywa katika misitu, halitatoa matokeo makubwa, na likielekezwa mijini, halipatani na kisingizio cha kupambana na mihadarati hivyo madai ya Marekani yataharibika; mbali na kwamba upinzani wa wananchi unaweza kuanzisha mgogoro wa muda mrefu.
Hujjatul-Islam Fazil Falawirjani aliongeza: Nchi za jirani pia zimepinga hatua hizi vikali, hata Gustavo Petro – rais wa Colombia – akizungumza kwa ukali na kumtaja Trump, alisema: “Mtu aliyehusika katika kesi za ufisadi anataka kututia hofu.” Akasisitiza kuwa anatakiwa ajifunze kutoka katika historia ya eneo hilo na mapambano ya wananchi. Kwa jumla, mambo haya yanaonesha kuwa suala la uvamizi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Venezuela si jambo rahisi na linaweza kuleta athari nzito kwa Marekani.
Maoni yako